Category: STORY

ILIKUWA WIKIENDI YA KIBABE LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC iliendelea mwishoni mwa wiki iliyopita kwa michezo mitatu iliyochezwa katika mikoa ya Lindi, Kagera na Dar es Salaam.

Namungo iliwakaribisha JKT Tanzania katika mchezo uliochezwa uwanja wa Majaliwa Ruangwa mkoani Lindi katika mchezo uliomalizika kwa suluhu.

Golikipa wa Namungo Jonathan Nahimana alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kufanikiwa kudhibiti mashambulizi yaliyolenga langoni kwake.

Katika mchezo uliochezwa siku ya jumamosi uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera timu ya Kagera Sugar iliikaribisha Simba majira ya saa kumi alasiri.

Simba ndio ilikuwa wa kwanza kutikisa nyavu za Kagera Sugar baada ya beki wa timu hiyo Shomari Kapombe kufunga bao la dakika ya 13 ya mchezo huo na baadae Jean Ahoua aliiongezea timu yake bao dakika ya 44 ya mchezo huo na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi timu zote zikishambuliana na dakika ya 53 ya mchezo huo kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma alifunga bao la tatu kwa kichwa baada ya mpira wa kona kupigwa na Ladack Chasambi.

Steven Mukwala aliongeza bao la nne kwa timu ya Simba akipokea pasi kutoka kwa Ladack Chasambi dakika ya 66 ya mchezo huo na Kagera Sugar ilipata bai kupitia Datius Peter dakika ya 79 na Mukwala alirudi tena kambani kwa Kagera dakika ya 84 na dakika chache baadae Cleophace Mkandala wa Kagera aliongeza bao hivyo mchezo kumalizika 2-5.

Kiungo wa Simba Jean Ahoua alitangazwa kuwa nyota wa mchezo huo kutokana na namna alivyoisaidia timu yake kupata ushindi.

Mchezo Mwingine ulichezwa siku ya jumapili katika uwanja wa KMC Complex mkoani Dar es Salaam timu ya Yanga ilikuwa mwenyeji wa Prisons kutoka Mbeya.

Dakika ya 13 ya mchezo huo mshambuliaji wa Yanga Clement Mzize alifungua ukurasa wa mabao na beki wa timu hiyo Ibrahim Hamad aliongeza bao la pili dakika ya 42 ya mchezo huku mshambuliaji Prince Dube akifunga dakika ya 45 hivyo kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Yanga ikishambulia zaidi na dakika ya 83 beki wa timu hiyo Ibrahim Hamad aliongeza bao la nne kwa timu yake hivyo kuifanya mechi kuisha 4-0.

Beki wa Yanga Ibrahim Hamad alitangazwa kuwa nyota wa mchezo huo baada ya kuisaidia timu yake kupata ushindi wa mabao manne huku yeye akifunga mabao mawili katika mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho kwa michezo miwili Simba watawakaribisha JKT Tanzania katika uwanja wa KMC huku Singida wakiwakaribisha Kengold uwanja wa CCM Liti.

ATEBA AIZAMISHA KENGOLD LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana katika uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kwa timu ya Simba kuwakaribisha wachimba dhahabu wa mkoani Mbeya timu ya KenGold saa 10:00 alasiri.

Dakika ya 34 ya mchezo huo mshambuliaji wa Simba Leonel Ateba alifunga goli kwa mkwaju wa penati baada ya kiungo wao Awesu Awesu kufanyiwa madhambi na mchezaji wa KenGold.

Ilimchukua dakika 10 Ateba kuiongezea bao timu yake akipokea pasi kutoka kwa beki wa kushoto Valentin Nouma aliyepiga kona hivyo kuifanya timu yao kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya Simba kushambulia kwa kasi lango la mpinzani wao hata hivyo walishindwa kutikisa nyavu za mpinzani wao baada ya kudhibitiwa vyema na mabeki wa KenGold na mchezo kutamatika kwa Simba kushinda 2-0.

Simba imefanikiwa kupanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Azam wenye alama 33 baada ya kufikisha alama 31 wakiishusha timu ya Singida Black Stars yenye alama 30.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo mkoani Dar es Salaam kwa mchezo mmoja ambapo timu ya Yanga itaikaribisha timu ya Mashujaa kutoka mkoani Kigoma saa 10:00 alasiri.

TABORA, COASTAL HAKUNA MBABE, AZAM IKITAMBA.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea jana kwa michezo miwili iliyochezwa katika mikoa ya Tabora na Dar es Salaam.

Mchezo uliochezwa mkoani Tabora timu ya Tabora United iliikaribisha timu ya Coastal Union katika mchezo uliochezwa saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kutamatika kwa sare ya 1-1.

Coastal Union ilianza kufunga bao kupitia kwa mchezaji Jeremiah Ntambwe aliyefunga katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na alikuwa mchezaji wa Tabora, Banele Sikhondze aliyefanikiwa kuweka sawa mzani baada ya kuipatia bao timu yake hivyo kufanya ubao kusomeka 1-1 mpaka mwisho wa mchezo huo.

Golikipa wa Tabora Hussein Masalanga alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na namna alivyoweza kulinda lango lake dhidi ya mashambulizi yaliyofanywa na Coastal Union.

Mchezo wa pili ulikuwa kati ya Azam na Fountain Gate kwenye uwanja wa Azam Complex na kumalizikwa kwa Azam kushinda kwa mabao 2-0.

Gibril Sillah ndio alianza kutikisa nyavu za Fountain Gate dakika ya 40 ya mchezo huo akipokea pasi kutoka kwa kiungo wa timu hiyo Feisal Salum hivyo kuwafanya Azam kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja.

Kocha wa Azam Rachid Taoussi alifanya mabadiliko kipindi cha pili cha mchezo huo na kumtambulisha mchezoni mshambuliaji Allasane Diao ambaye amerejea baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.

Allasane aliiongezea bao timu yake hivyo kuifanya Azam kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya kufikisha alama 33 na Kiungo wa Azam Feisal Salum alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa mchezo mmoja utakaochezwa uwanja wa KMC Complex kati ya Simba na KenGold kutoka jijini Mbeya saa 10:00 alasiri.

TABORA, COASTAL KUKIWASHA LEO, AZAM KUJIULIZA NYUMBANI.

TIMU ya Tabora United iliyopo kwenye muendelezo mzuri wa matokeo leo inashuka dimbani kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora dhidi ya Coastal union ya Tanga saa 10:00 alasiri.

Tabora inaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata matokeo ya ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wake uliopita nyumbani dhidi ya Azam ya Dar es Salaam.

Coastal inakutana na Tabora ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya Fountain kwa mabao 3-2 kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.

Mchezo wa mwisho leo utakuwa kati ya Azam FC dhidi ya Fountain Gate FC kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar saa 1:00 usiku.

Azam itajaribu kupata ushindi leo ikiwa ni baada ya kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya Tabora United huku Fountain ikijaribu kuendeleza matokeo mazuri ya ushindi baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Coastal nyumbani.

DODOMA YASHINDWA KUTAMBA, KMC IKIBANWA

LIGI Kuu ya NBC imeendelea katika viwanja vya CCM Liti mkoani Singida na KMC Complex mkoani Dar es Salaam kwa michezo iliyochezwa saa 8:00 mchana na saa 10:00 alasiri.

Ilichukua dakika nane pekee kwa mshambuliaji wa Singida Black Stars Elvis Rupia kufungua ubao wa mabao kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 15 hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 58 Dodoma Jiji walifanikiwa kupata bao kupitia mchezaji wao Yassin Mgaza na kufanya ubao wa mabao kusomeka 2-1 mpaka mwisho wa mchezo huo.

Elvis Rupia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kiwango kizuri alichoonyesha na kuisaidia timu yake kupata ushindi.

Mchezo wa pili KMC iliikaribisha Mashujaa huku timu zote zikishambuliana kwa kasi hata hivyo ulimalizika kwa suluhu na mchezaji wa Mashujaa Kalos Protas alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.