Category: STORY

‘WAZEE’ WA ‘MAKOMBORA’ YA LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 imeendelea kushuhudia mabao ya kuvutia kutoka nje ya eneo la hatari, huku baadhi ya nyota wakionyesha uwezo mkubwa wa kupiga mashuti sahihi yanayowapa mashabiki burudani ya kipekee.

Kinara wa orodha hiyo ni mshambuliaji wa Azam Idd Seleman ambaye hadi sasa ameweka kambani mabao matano akifunga kutoka nje ya eneo la 18 ambapo wezo wake wa kupiga mashuti ya kushtukiza umekuwa silaha muhimu kwa Azam katika harakati za kutafuta mafanikio msimu huu.

Nafasi ya pili inashikiliwa na kiungo mshambuliaji wa Simba Clatous Chama aliyefunga mabao manne kutoka nje ya eneo la 18.

Chama ameendelea kuthibitisha ubora wake wa muda mrefu kwa kutengeneza nafasi na kufunga mabao muhimu katika nyakati ngumu za mchezo zinazowafanya Simba kuendelea kusalia kwenye mbio za ubingwa.

Katika nafasi ya tatu ni nyota wa Mtibwa Sugar Ismail Mhesa, mwenye mabao matatu ya nje ya boksi likiwemo lile alilofunga kwa mpira wa kona ulioingia moja kwa moja dhidi ya Young Africans.

Beki wa Singida Black Stars, Ibrahim Imoro ambaye licha ya kucheza nafasi ya ulinzi amekuwa tishio kubwa kupitia mashuti yake ya mbali na mipira ya adhabu nae amefunga matatu sawa na Mhesa.

Kadri msimu unavyoelekea ukingoni mashabiki wataendelea kutarajia kuona mabao mengi zaidi ya kuvutia kutoka kwa nyota hawa wenye uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo kwa shuti moja tu lililo sahihi.

OKELLO KINARA WA MABAO YA MGUU WA KUSHOTO LIGI KUU YA NBC.

 

MSHAMBULIAJI wa Young Africans raia wa Uganda Allan Okello ameendelea kuonyesha ubora wake katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 baada ya kuongoza kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwa kutumia mguu wa kushoto.

Nyota huyo anaongoza kwa mabao 10 ya mguu wa kushoto akithibitisha uwezo wake mkubwa wa kumalizia mashambulizi na kuwa silaha muhimu kwa Young Africans katika harakati za kutetea ubingwa wao.

Nyuma yake wapo nyota wawili waliolingana kwa mabao sita kila mmoja ambao ni Libasse Guèye wa Simba na Salehe Karabaka wa JKT waliotoa mchango mkubwa katika safu za ushambuliaji za timu zao.

Katika nafasi ya nne ni Fredrick Magata wa Mtibwa Sugar mwenye mabao matano ya mguu wa kushoto huku Methew Tegisi wa Pamba Jiji akifuatia kwa mabao manne.

Wachezaji wengine waliopo kwenye orodha hiyo ni Selemani Mwalimu, Clatous Chama wa Simba na Prince Dube wa Young africans waliofunga mabao manne kwa kutumia mguu wao wa kushoto kila mmoja.

Hii inaonyesha umuhimu wa wachezaji wenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto kwa ufanisi huku Allan Okello akiendelea kuwa kinara na mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa zaidi kwa ‘wananchi’ katika mashindano ya Ligi Kuu ya NBC.

GEITA ‘WAKALI’ WA KUTUPIA NBC CHAMPIONSHIP.

Geita Gold imeendelea kuonyesha ‘ubabe’ wake kwenye Ligi ya Championship ya NBC baada ya kutupia mabao 60 ikiwa ni idadi kubwa hadi sasa msimu wa 2025/2026.

Timu hiyo iliyopo katika mbio za kurejea Ligi Kuu ya NBC baada ya kushuka msimu wa 2023/2024 ikiwa ni takribani misimu miwili ikicheza Ligi ya Championship huku ikiongoza msimamo na alama 68.

Mbeya Kwanza nayo haiko nyuma ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi hiyo imeweza kutikisa nyavu za wapinzani wake mara 51.

Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo imeweza kufunga mabao 49 ikiwa ni timu ya tatu kwa kufunga mabao mengi zaidi ndani ya Championship.

Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro ipo nafasi ya tatu kwa timu zenye mabao mengi ambapo imefunga mabao 47 yanayoiweka katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Transit Camp haipo mbali ikiwa imetikisa nyavu za wapinzani wao mara 38 huku ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Kwa upande wa ‘wajeda’ wa Mbuni wenye maskani yake mkoani Arusha imefanikiwa kufunga mabao 36 ndani ya Ligi hiyo huku ikiwa nafasi ya sita katika msimamo.

CHIRWA HAKAMATIKI NBC CHAMPIONSHIP.

MSHAMBULIAJI wa timu ya Kagera Sugar Obrey Chirwa hakamatiki hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuwa kinara kwa kufunga mabao akiwa nayo 16 hadi sasa ndani ya Ligi ya Championship ya NBC.

Ligi hiyo imeshachezwa mizunguko 27 huku ikiwa imesalia mizunguko mitatu ili Ligi hiyo kufikia ukingoni ambapo pia mchezaji huyo ameisaidia timu yake kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwania kurejea Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 65.

Maulid Shaban wa Geita Gold hayupo mbali akiwa amefanikiwa kuifungia mabao 14 timu yake ambayo ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikikusanya alama 68.

Ramadhani Kalanje wa timu ya B19 nae ameweza kutikisa nyavu za wapinzani wao mara 13 huku timu hiyo ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo ikikusanya alama 31.

Abdereheman Mussa wa Transit Camp iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo na Emmanuel Mpuka wa Polisi Tanzania iliyopo nafasi ya tatu wameweza kufunga mabao 12 kila mmoja.

Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp kabla ya kuhamia KMC ya Ligi Kuu ya NBC, Boniface Brown wa Mbeya Kwanza na Samson Kassian wa KenGold wamefanikiwa kufunga mabao 11 kila mmoja hadi sasa kwenye ligi hiyo.

‘WALINDA LANGO’ LA AZAM NI MOTO WA KUOTEA MBALI LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 imeendelea kushuhudia ushindani mkubwa si tu katika ufungaji wa mabao, bali pia katika uimara wa safu za ulinzi huku takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Azam ndiyo timu iliyocheza michezo mingi zaidi bila kuruhusu bao, ikifanikiwa kutofungwa katika michezo 20 hadi sasa.

Azam imeonyesha nidhamu kubwa langoni chini ya magolikipa wao Aishi Manula aliyecheza michezo 11 bila kuruhusu bao, Zuberi Foba aliyecheza michezo nane bila kuruhusu na Issa Fofana aliyefanya hivyo kwenye mchezo mmoja.

Mabingwa watetezi Young Africans wanafuatia kwa kutofungwa bao katika michezo 19 wakionyesha uimara mkubwa wa walinda mlango wao chini ya Djigui Diarra, Hussein Masalanga na Abutwalib Mshery.

Simba wanashika nafasi ya tatu kwa michezo 17 ya kutofungwa bao, huku Mashujaa wakishika nafasi ya nne kwa michezo 12, Dodoma Jiji wakikusanya michezo 11 ya kutofungwa bao na kujikita miongoni mwa timu zenye safu bora za golikipa msimu huu.

JKT Tanzania, TRA na Pamba Jiji zote zimefanikiwa kutofungwa bao katika michezo 10 kila moja, zikithibitisha uimara wao wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya wapinzani.

Orodha hii inaonyesha wazi kuwa mafanikio ya timu nyingi msimu huu hayajatokana na ushambuliaji pekee, bali pia uimara wa walinda mlango na mabeki ambao wamekuwa nguzo muhimu katika kupambania matokeo chanya ndani ya Ligi Kuu ya NBC.