Tag: #LIGIKUU #NBCPL #COASTALUNION #JKTTANZANIA

DUKE,PEDRO WANG’ARA TUZO ZA DISEMBA

MCHEZAJI Duke Abuya wa Klabu ya Young Africans, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Disemba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku Pedro Goncalves pia wa Young Africans akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa Ligi hiyo kwa mwezi huo.

Duke alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiisaidia timu yake kushinda michezo miwili iliyocheza mwezi huo, pamoja na kuhusika katika mabao mawili kwa dakika 180 za michezo hiyo.

Mchezaji huyo aliwashinda Nassor Saadun wa Azam na Prince Dube wa Young Africans alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa upande wa Pedro aliyeingia fainali katika mchakato huo na Florent Ibenge wa Azam na Etienne Ndairagije wa TRA United, aliiongoza timu yake kushinda michezo miwili na kupaa kutoka nafasi ya nne hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo. Young Africans ilizifunga Fountain Gate (2-0), na Coastal Union (0-1).

Wakati huohuo Meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Said Mpuche, amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Disemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Mchezaji wa Transit Camp Adam Uledi

Katika hatua nyingine mchezaji wa Transit Camp, Adam Uledi, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Disemba wa Ligi ya Championship ya NBC 2025/26, huku Shadrack Nsajigwa pia wa Transit Camp akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Uledi aliyeingia fainali katika mchakato huo na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar na Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza, alionesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kucheza dakika 450 za michezo mitano aliyocheza.

Kwa upande wa Nsajigwa aliyeingia fainali na Juma Kaseja wa Kagera Sugar na Zuberi Katwila wa Geita Gold aliiwezesha timu yake kushinda michezo yote mitano iliyocheza mwezi huo.

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

TAARIFA YA KAMATI YA UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB)

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Julai 15, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 229: KenGold FC 0-5 Simba SC

Timu ya KenGold ya mkoani Mbeya imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuingia kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kuelekea mchezo tajwa hapo juu Juni 18,2025.KenGold iliingia uwanjani saa 9:35 alasiri badala ya saa 8:30 mchana jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 231: Azam FC 5-0 Tabora United FC

Klabu ya Tabora United imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kushindwa kuhudhuria mkutano wa wanahabari kwenye ukumbi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Juni 17, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:58 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 184: Young Africans SC 2-0 Simba SC

Klabu ya Simba imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kushindwa kuhudhuria mkutano wa wanahabari kwenye ukumbi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Juni 24, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:58 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Klabu ya Simba imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) Juni 24, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Klabu ya Simba imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kuingia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo tajwa hapo juu Juni 25, 2025, kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:21 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Michezo ya Mtoano (Play-Off) Hadhi ya Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba PO1: Stand United 1-3 Fountain Gate

Klabu ya Fountain Gate imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kikosi chake kulazimisha kupita katika eneo lililotengwa na kuwekewa uzio kwa ajili ya shughuli ya uzalishaji maudhui ya mchezo huo inayofanywa na mdhamini mwenye haki za matangazo ya runinga, Azam Media Limited.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Fountain Gate imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Stand United imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake kumrushia mawe mwamuzi msaidizi namba moja wa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga Julai 4, 2025.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Wachezaji Edgar Williams (Fountain Gate) na Selemani Richard Seif (Stand United) wamefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kila mmoja kwakosa la kukataa kuingia kwenye vyumba vya kuvalia wakati wa mapumziko na kusalia kiwanjani.

Wachezaji hao wawili walionekana kutegeana kila mmoja akisubiri mwenzake awe wakwanza kuondoka kiwanjani jambo ambalo lilileta picha mbaya iliyotafsiriwa kama kitendokinachoashiria Imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 41:5(5.5) ya Ligi Kuu na Kanuni ya 41:5(5.5) yaChampionship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Shauri la Uhalali wa Wachezaji wa Tunduru Korosho

Timu ya Tunduru Korosho ya mkoani Ruvuma imetozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) na kuporwa ushindi wa jumla wa michezo miwili ya hatua ya mtoano dhidi ya Cargo FC ya Dar es Salaa, kuwania hadhi ya kucheza First League msimu wa 2025/2026 na timu ya Cargo kupewa ushindi pamoja na kupandishwa daraja kwenda First League 2025/2026, baada ya timu ya Tunduru kuthibitika iliwatumia wachezaji wawili ambao haikuwasajili.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 48:23 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Kocha mkuu wa klabu ya Tunduru Korosho, Ramadhan Kadunda amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuwachezesha wachezaji wawili ambao hawakusajiliwa na klabu hiyo kwa ajili ya msimu wa 2024/2025.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 46:2(2.10) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Katibu mkuu wa klabu ya Tunduru Korosho, Hassan Issa amepelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa tuhuma za kughushi nyaraka za TFF zikiwemo leseni za wachezaji wawili waliotumika katika michezo tajwa hapo juu isivyo kihalali.Mratibu (GC) wa mchezo tajwa hapo juu,Mkwenya Manya amepelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kuchelewa kwa makusudi kutuma nyaraka (picha za leseni za wachezaji) zilizoombwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, jambo ambalo limetafsiriwa kama hila za kuficha udanganyifu uliofanywa na klabu ya Tunduru Korosho.

Wachezaji Miraji Mohamed Daud na Oscar Stuati Omari wa klabu ya TANESCO ya mkoani Iringa, wamefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kosa la kuitumikia klabu yaTunduru Korosho katika michezo ya hatua ya mtoano wakiwa wanafahamu kuwa wao si wachezaji halali wa klabu hiyo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 48:23 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Imetolewa na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

Julai 17, 2025

MTIBWA SUGAR MABINGWA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC 2024/2025.

TIMU ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/2025.

Mtibwa Sugar kwenye mchezo wake wa mwisho hii Leo dhidi ya Kiluvya iliyochezwa kwenye uwanja wa Manungu Complex imefanikiwa kuibuka na kushinda wa mabao 2-0 myaliyofungwa na Raizin Hafidh dakika ya 36 na 46 ya mchezo huo.

Baada ya ushindi huo Mtibwa Sugar inafikisha alama 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote inayoshiriki Ligi ya Championship ya NBC.

Mtibwa Sugar ambayo ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita imefanikiwa kufunga mabao 58 huku ikifungwa mabao 18 hivyo kujihakikisha nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026.

LIGI KUU YA NBC

LIGI KUU YA NBC KUCHEZWA ARUSHA, SINGIDA LEO.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Februari 7, 2025 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Arusha na Singida kuanzia saa 10:00 Alasiri.

Mkoani Arusha Coastal Union itaikaribisha JKT Tanzania kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku ikiingia kwenye mchezo huu ikishika nafasi ya 11 ikikusanya alama 18 kwenye michezo 16 na JKT Tanzania ikishika nafasi ya nane baada ya kukusanya alama 19 wakiwa na tofauti ya alama moja (1) pekee kati yao.

Mkoani Singida, timu ya Singida Black Stars itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar ya mkoani Kagera kwenye uwanja wa CCM Liti huku mara ya mwisho timu hizi kukutana Agosti 24, 2024 mkoani Kagera, Singida Black Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Mchezaji Anthony Tra Bi dakika ya 90+3 ya mchezo huo.

Michezo hii miwili inakamilisha michezo ya mzunguko wa 17 wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 ambapo mpaka sasa timu ya Young Africans ikishika usukani na alama 45 huku Kengold ikiburuza mkia ikiwa na alama sita pekee.

 

LIGI KUU NBC YA NNE KWA UBORA AFRIKA

Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu ya Tanzania (NBC Premier League) kuwa Ligi ya nne kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024.

Ligi hiyo imepanda kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya sita mwaka 2023 hadi nafasi ya nne ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia.

Kwa mujibu wa taarifa ya IFFHS kwa upande wa Afrika nchi zilizoko chini ya Shirikisho la Soka (CAF) Ligi Kuu ya Misri inayofahamika kama Nile Premier League ndio kinara kwa ubora Afrika.

Nafasi ya pili inashikiliwa na Botola Pro ambayo ni Ligi Kuu ya Morocco huku League 1 ya Algeria ikishika nafasi ya tatu kwa ubora mwaka 2024.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania imekwea hadi nafasi ya nne barani Afrika kutokana na ligi hiyo kuwa na usimamizi bora kuanzia Serikali, Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Klabu zinazoshiriki ligi hiyo, wadhamini mbalimbali wanavyounga mkono pamoja na mashabiki.