Author: Loveness Bernard

LIGI KUU NBC KUREJEA WIKIENDI .

Ligi Kuu ya NBC ligi ya nne kwa ubora barani Afrika inarejea wikiendi hii febuari 1 baada ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja .

Ligi hiyo itaanza kwa michezo miwili ya viporo vya mzunguko wa 16 ambavyo ni mechi za Yanga dhidi ya Kagera Sugar Februari 1 katika uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam.

Februari 2 Tabora United itakuwa mwenyeji wa Simba katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora katika mchezo uliokuwa umepangiwa tarehe mpya.

Mzunguko wa 17 utaanza rasmi februari tano hadi saba kwa michezo nane itakayochezwa katika viwanja mbalimbali nchini .

Akizungumza kuhusu kurejea kwa Ligi Afisa Habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda amesema kuwa maandalizi yote yako tayari na kwa upande wa usimamizi Bodi iko tayari, timu, viwanja vimekaguliwa ubora wake viko na upande wa ratiba ilishatoka mapema” Amesema Boimanda na kuongeza kuwa

“Mapumziko ya Ligi yalitokana na uwepo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa mwanzoni mwa mwezi januari kisiwani Pemba na pia uwepo wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani yaani CHAN ambazo zilipaswa kufanyika februari kabla ya kusogezwa mbele hadi agosti 2 ambapo Tanzania,Kenya na Uganda ni nchi zinazoandaa michuano hiyo”.

STAND YAILIZA KILUVYA,MBUNI YAJIPATA KWA POLISI NBC CHAMPIONSHIP

LIGI ya NBC Championship Mzunguko wa 16 leo imeendelea kwa michezo minne ya mwisho ya mzunguko huo iliyochezwa viwanja mbalimbali nchini  kuanzia majira ya saa nne  asubuhi  na saa kumi jioni.

Bigman waliwakaribisha Mbeya City katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi saa nne asubuhi baada ya mchezo huo kuahirishwa kuchezwa jana kutokana na mvua iliyonyesha mkoani Lindi  na kusababisha uwanja kujaa maji.

Katika mchezo huo Bigman walifanikiwa kuchukua alama 3 kutoka kwa Mbeya City na kufikisha alama 25 katika msimamo wa Ligi hiyo wakiwa nafasi ya saba  baada ya mchezaji wao Francis Kapeta kufunga bao pekee kwa mkwaju wa penati hivyo mchezo kumalizika 1-0.

Mchezo mwingine ulichezwa majira ya saa kumi jioni ambapo timu ya Stand United waliwakaribisha timu ya Kiluvya katika uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Dakika ya saba ya mchezo huo Stand United walifungua akaunti ya mabao kupitia mchezaji wao Lukas Sendama na dakika kumi baadae Adam Uledi aliongeza bao la pili hivyo kuwafanya Stand United kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao mawili.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Kiluvya walifanikiwa kupata bao dakika ya 66 ya mchezo huo kupitia mchezaji wao Hassan Bundala na dakika ya 82 Sendama alirudi tena nyavuni hivyo kuwafanya Stand United kuchukua alama zote tatu na mchezo kumalizika kwa 3-1, Stand United wamepanda hadi nafasi ya nne wakiwa na alama 32.

Kwa upande wa mechi ya Mbuni dhidi ya  timu ya Polisi Tanzania iliyochezwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha mechi ilianza saa kumi alasiri.

Katika mchezo huo Mbuni walifanikiwa kupata bao dakika ya 33 ya mchezo huo kupitia mchezaji Malulu Thomas kabla ya Hassan Rishedy kuongeza bao la pili dakika ya 44 hivyo Mbuni  hivyo matokeo kubaki hivyo hadi mwisho wa mchezo huo  2-0 hivyo kufikisha alama 23 huku wakiwa nafasi ya tisa kakika msimamo.

Timu ya Transit Camp waliwakaribisha  timu ya Biashara United kutoka mkoani Mara kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi Mkoani Pwani

Katika mchezo huo Biashara United walifanikiwa kubeba alama tatu baada ya mchezaji wao Timotheo Abubakar kufunga bao dakika ya 28 ya mchezo huo ambao ulitamatika  kwa matokeo ya 0-1 hivyo Biashara kufanikiwa kupata alama tatu mhimu wakifikisha alama 4 huku wakiwa wa mwisho katika msimamo wa Ligi hiyo.

TMA YAJIPATA KWA GEITA GOLD NBC CHAMPIONSHIP

LIGI ya NBC Championship Mzunguko wa 16 ulianza jana januari 24 kwa michezo ilicho  na leo imeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa mkoani Arusha Katika Uwanja wa Sheikh Amri  Abeid majira ya  saa kumi jioni.

Katika mchezo huo timu ya TMA waliwakaribisha Geita Gold ambapo mchezo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa kasi  kubwa ambapo mpaka mapumziko hakuna aliyeweza kutikisa nyavu za mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa ambapo TMA walifanikiwa kupata bao la kwanza ikiwa ni dakika ya 50 ya mchezo huo  kupitia mchezaji wao Abdul Shahame kabla ya Kasimu Shaibu kuongeza bao  la pili dakika ya 61 ya mchezo huo .

Dakika ya 72 ya mchezo huo Geita Gold walifanikiwa kupata goli lao la kwanza kupitia mchezaji wao Masanja Jesto  hivyo matokeo kuwa 2-1 ambayo yalisalia mpaka mwisho wa mchezo huo.

Baada ya mchezo huo kutamatika TMA alifanikiwa kufikisha pointi 30 hivyo kupanda hadi nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi hiyo kutoka nafasi ya sita alipokuwa awali.

Ligi ya NBC Championship itaendelea kesho kwa michezo minne Bigman dhidi ya Mbeya City ulioahirishwa kuchezwa leo kutokana na mvua kubwa kunyesha katika uwanja wa Ilulu Lindi,Stand United dhidi ya Kiluvya,Transit Camp dhidi ya Biashara United na Mbuni dhidi ya Polisi Tanzania.

LIGI KUU NBC YA NNE KWA UBORA AFRIKA

Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu ya Tanzania (NBC Premier League) kuwa Ligi ya nne kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024.

Ligi hiyo imepanda kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya sita mwaka 2023 hadi nafasi ya nne ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia.

Kwa mujibu wa taarifa ya IFFHS kwa upande wa Afrika nchi zilizoko chini ya Shirikisho la Soka (CAF) Ligi Kuu ya Misri inayofahamika kama Nile Premier League ndio kinara kwa ubora Afrika.

Nafasi ya pili inashikiliwa na Botola Pro ambayo ni Ligi Kuu ya Morocco huku League 1 ya Algeria ikishika nafasi ya tatu kwa ubora mwaka 2024.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania imekwea hadi nafasi ya nne barani Afrika kutokana na ligi hiyo kuwa na usimamizi bora kuanzia Serikali, Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Klabu zinazoshiriki ligi hiyo, wadhamini mbalimbali wanavyounga mkono pamoja na mashabiki.

HAWA HAPA WASHINDI WA TUZO ZA NBC DESEMBA.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Desemba wa Ligi Kuu ya NBC huku Kocha wa Yanga Sead Ramovic akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.

Mzize amewashinda Prince Dube wa Yanga na Feisal Salum wa Azam alioingia nao fainali za tuzo hizo baada ya kufunga mabao 4 na kutoa pasi za mwisho 3 katika dakika 288 alizocheza ndani ya mwezi huo.

Yanga ilizifunga Tanzania Prisons mabao 4-0, Dodoma Jiji 0-4 Mashujaa 3-2, na Fountain Gate mabao 5-0 hivyo kukusanya alama 12.

Aidha Kocha wa Yanga Sead Ramovic amefanikiwa kuwa kocha Bora wa mwezi huo baada ya kuwashinda Davis Fadlu wa Simba na Rachid Taoussi wa Azam baada ya kuiongoza Yanga kushinda michezo minne ambayo timu yake ilicheza ndani ya mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Kamati ya Tuzo pia imemchagua Meneja wa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Dar es Salaam, Ashraf Omar kuwa Meneja bora wa uwanja mwezi desemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo na masuala ya miundombinu.

Kwa upande wa Ligi ya Championship ya NBC kamati imemchagua mchezaji wa Mbeya City, Kilaza Mazoea kuwa mchezaji bora wa Ligi hiyo kwa mwezi desemba baada ya kufunga mabao manne katika dakika 234 alizocheza akiwashinda Elias Maguri wa Geita Gold/Biashara na Emmanuel Maziku wa Stand United.

Kocha wa Mbeya City Salum Mayanga, amechaguliwa kuwa kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi desemba ambapo aliiongoza timu yake kushinda michezo 3 na kufanikiwa kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo akiwashinda Awadh Juma wa Mtibwa na Maka Mwalwisi wa TMA alioingia nao fainali.

Mbeya City walizifunga timu za Polisi Tanzania 4-0,Geita Gold 1-0 na Cosmopolitan 1-0.