Tag: #LIGIKUU #NBCPL #AZAM #YANGA #SIMBA #KMC #JKT #MASHUJAA #KENGOLD #DODOMAJIJI #PAMBAJIJI #KAGERASUGAR #SINGIDABLACKSTARS #FOUNTAINGATE #NAMUNGO

LIGI KUU NBC KAZINI VIWANJA VINNE LEO.

BAADA ya kupigwa michezo miwili jana Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo kwa michezo minne ya mzunguko wa 28 katika viwanja vinne tofauti .

Mchezo wa kwanza utapigwa majira ya saa 8:00 mchana katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni Dar es Salaam ambapo JKT Tanzania itaikaribisha timu ya Fountain Gate kutoka Manyara.

Saa 10:00 alasiri itapigwa michezo miwili ambapo mchezo wa kwanza ni kati ya Young Africans ikiwaalika Namungo katika uwanja wa KMC Complex mkoani Dar es Salaam na KenGold itaikaribisha Pamba Jiji katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Mchezo wa mwisho utachezwa saa 1:00 usiku ambapo timu ya Azam itakuwa mwenyeji wa timu ya Dodoma Jiji katika uwanja wa Azam Complex, Dar.

KAGERA SUGAR ‘HATIHATI’ KUSHIRIKI LIGI KUU YA NBC MSIMU UJAO.

MATUMAINI ya wapenzi na mashabiki wa timu ya Kagera Sugar kusalia Ligi Kuu ya NBC yamezidi kufifia baada ya kufungwa na timu ya Mashujaa katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera jana kwa bao 1-0.

Timu hiyo imeshacheza michezo 28 ya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/25 na kufanikiwa kuvuna alama 22 ikifunga mabao 22 na kuruhusu mabao 40 huku ikiwa imebakisha michezo miwili kumaliza msimu.

Aidha timu hiyo endapo ikishinda michezo yote iliyobakia itaweza kufikisha alama 28 ikiwa ni tofauti ya alama moja na Pamba Jiji ambayo ina alama 27 ikifunga mabao 18 na kufungwa mabao 32 huku ikiwa imebaki michezo mitatu mkononi.

Endapo Pamba Jiji itashinda mchezo wa leo dhidi ya KenGold rasmi Kagera Sugar itashuka daraja na kushiriki Ligi ya Championship ya NBC.

PRISONS YATAKATA SOKOINE LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea mkoani Mbeya ambapo timu ya Tanzania Prisons iliikaribisha timu ya Coastal Union katika uwanja wa Sokoine na kukusanya alama zote tatu baada ya ushindi wa 2-1.

Mchezo huo ulianza saa 10:00 alasiri timu zote zilionyesha ari ya kupambania alama tatu muhimu ili kuweza kujiweka katika mazingira ya kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

Iliwachukua dakika 27 timu ya Tanzania Prisons kufungua ukurasa wa mabao kupitia mchezaji wao Ezekia Mwashilindi hivyo kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa 1-0.

Kipindi cha pili kilianza ambapo Coastal Union walionekana kuliandama zaidi lango la Prisons hata hivyo juhudi zao zilizimwa na mchezaji Beno Ngasa aliyeongeza bao la pili kwa timu yake dakika ya 74.

Dakika ya 89 Coastal Union ilipata bao la kufutia machozi kupitia mchezaji wao Bakari Msimu hivyo mchezo kutamatika kwa matokeo ya 2-1.

Tanzania Prisons ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imevuna alama 30 katika michezo 28 huku Coastal Union ikiwa nafasi ya 9 na alama 31 katika michezo 28 ya Ligi Kuu msimu wa 2024/2025.

CAMARA MKALI WA ‘HATI SAFI’ LIGI KUU YA NBC.

GOLIKIPA wa timu ya Simba, Moussa Camara ameendeleza moto wake wa kuongoza kwa kuwa na hati safi nyingi kuliko magolikipa wengine wa timu za Ligi Kuu ya NBC akiwa hajaruhusu bao kwenye michezo 16 akiwa kwenye msimu wa kwanza ndani ya Simba.

Camara mpaka sasa amecheza michezo 24 sawa na dakika 2160 huku timu yake ya Simba ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Young Africans inayoshikilia usukani.

Golikipa wa Young Africans,Djigui Diarra anafuatia akiwa amecheza dakika 1819 katika michezo 20 ya Ligi Kuu ya NBC amefanikiwa kukusanya hati safi 14.

Patrick Munthali wa timu ya Mashujaa kutoka Kigoma anashika nafasi ya tatu akiwa amefanikiwa kukusanya hati safi 12 huku Mohamed Mustapha wa timu ya Azam akishika nafasi ya nne na hati safi 10.

Nafasi ya tano inashikiliwa na Yona Amos wa Pamba Jiji aliyefanikiwa kukusanya hati safi tisa huku Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania amekusanya hati nane akishika nafasi ya sita.

Metacha Mnata wa Singida Black Stars na Ngaleka Katembua wa Dodoma Jiji wanafunga orodha wakifanikiwa kukusanya hati safi saba kila mmoja.

NYASI ‘KUWAKA’ MOTO LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC leo inatimua vumbi kwa michezo miwili itakayopigwa kwenye viwanja vya Sokoine, Mbeya na Kaitaba, Kagera.

Mchezo wa saa 10:00 alasiri utakuwa kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Coastal Union ambapo Prisons inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kujiondoa kwenye nafasi ya kucheza michezo ya mtoano.

Endapo Prisons inayoshika nafasi ya 14 itashinda itafikisha alama 30 na itakuwa nyuma ya Coastal Union inayoshika nafasi ya nane kwa tofauti ya alama moja pekee.

Mchezo wa mwisho utapigwa mkoani Kagera kwenye uwanja wa Kaitaba saa 12:30 jioni kati ya Kagera Sugar dhidi ya Mashujaa.

Kagera inayoshika nafasi ya 14 inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kufufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu 2025/26 huku Mashujaa ikihitaji alama tatu muhimu kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye ligi hiyo.