Category: STORY

HAUSUNG, RHINO VINARA MBIO ZA KUPANDA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

LIGI ya First League inazidi kupamba moto kwenye viwanja tofauti huku timu za Hausang ya Makambako Njombe na Rhino Rangers ya Tabora zikiongoza mbio hizo.

Timu ya Hausang inaongoza kundi A baada ya kucheza michezo 12 ikishinda michezo sita, sare nne na kupoteza miwili huku ikifanikiwa kukusanya alama 22.

Timu ya Magnet inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na alama 11 baada ya kushinda michezo miwili, kupoteza mitano na sare tano.

Rhino Rangers inashikilia usukani wa kundi B ikikusanya alama 28 baada ya kushinda michezo tisa, sare mchezo mmoja na kupoteza michezo miwili.

Rhino inaongoza pia kwenye kupachika mabao ikifunga (30) huku Ruvu Shooting ikiwa timu iliyofunga mabao machache hadi sasa ikifunga mawili pekee.

Kinara wa kundi A atakutana na kinara wa kundi B katika mchezo wa mwisho wa msimu ili kumpata bingwa wa Ligi ya First League msimu wa 2024/25.

FEISAL MKALI WA ‘KUPIKA MABAO’ LIGI KUU YA NBC

KIUNGO wa Azam,Feisal Salum ameendelea kuwa kinara wa kupika mabao katika Ligi Kuu ya NBC kutokana na kuweza kutoa pasi 12 za mwisho kwa msimu wa 2024/2025 katika michezo 23 ambayo timu yake imeshacheza mpaka sasa akivunja rekodi ya msimu uliopita ambapo  Kipre Junior alimaliza na asisti 9.

Feisal ametoa pasi za mwisho katika michezo ya Azam dhidi za Namungo (1),JKT Tanzania (2),Fountain Gate (1),Coastal Union (1),Simba dhidi ya Azam (1),Azam dhidi ya KMC (1)  Tabora dhidi ya Azam (1).

Mechi zingine ambazo Feitoto ameweza kutoa pasi za mwishi ni  Dodoma Jiji dhidi ya Azam (1), Namungo dhidi ya Azam (1), KMC dhidi ya Azam (2).

Ukiachana na Feisal wachezaji Jean Ahoua wa Simba,Max Nzegeli ,Aziz Ki na Prince Dube wa Young Africans wamefanikiwa kutoa pasi za mwisho  saba kila mmoja.

AHOUA HASHIKIKI VITA YA UFUNGAJI BORA LIGI KUU NBC

HASHIKIKI  hivyo ndivyo unavyoweza  kusema kutokana na Kiungo mshambuliaji wa  timu ya Simba,Jean Ahoua, kutokana na mchezaji huyo kuwa na namba nzuri za mabao ndani ya  Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu wa 2024/2025.

Ikiwa ni msimu wake wa kwanza  ndani ya Simba akitokea nchini kwao Ivory Coast mchezaji huyo amefanikiwa kufunga mabao 12  kati ya mabao 52 ambayo timu ya Simba imefunga katika michezo 22 hadi sasa huku akifuatiwa na Clement Mzize mwenye mabao 10 sawa na Prince Dube ambao ni wachezaji Young African.

Ahoua amefunga mabao katika michezo ya Simba dhidi ya timu za Fountain Gate (1), Dodoma Jiji (1), Namungo (1), KMC (2), Kagera Sugar (1), JKT Tanzania (1), Tanzania Prisons (1), Namungo dhidi ya Simba (2) na Simba dhidi ya Dodoma Jiji (2).

Ahoua amekuwa na msimu mzuri kwenye Ligi Kuu ya NBC akishika nafasi ya tatu kwenye vinara wa pasi za mabao baada ya kutoa pasi saba hadi sasa.

STAND UNITED

NI VITA YA ‘TOP FOUR’ NBC CHAMPIONSHIP LEO.

MICHEZO mitatu ya Ligi ya Championship ya NBC inapigwa leo Machi 17 ambapo mikoa ya Geita, Mbeya na Shinyanga itakuwa wenyeji wa michezo hiyo.

Michezo ya Leo inazikutanisha baadhi ya timu zinazopambana kujiweka vizuri kwenye nafasi nne za juu za msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Stand United iliyo nafasi ya tatu na alama 46 itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar iliyo nafasi ya kwanza na alama 54 kwenye uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Mkoani Geita, Geita Gold inayoshika nafasi ya nne ikiwa na alama 45 itakuwa mwenyeji wa Mbeya Kwanza iliyo nafasi ya sita na alama 39 kwenye uwanja wa Nyankumbu.

Mchezo wa Mwisho leo utazikutanisha Mbeya City inayoshika nafasi ya pili dhidi ya Kiluvya iliyo nafasi ya 12 kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya huku michezo yote ya Leo itaanza kuanzia majira ya saa 10:00 za alasiri.

SIMBA KUWAVAA DODOMA LEO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaozikutanisha timu za Simba dhidi ya Dodoma kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar.

Simba iliyoshinda mchezo wake wa Ligi Kuu ya NBC uliopita ugenini dhidi ya Coastal Union kwa mabao 3-0 inakutana na Dodoma Jiji iliyolazimishawa suluhu na Coastal kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Timu ya Simba inahitaji alama tatu leo ili kujiweka nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa NBC msimu huu huku Dodoma ikihitaji kupata ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

Mchezo huu ni wa kiporo ulioahirishwa baada ya timu ya Dodoma Jiji kupata ajali ya basi ilipokuwa ikitoka mkoani Lindi baada ya mchezo dhidi ya Namungo kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi.