Category: STORY

FAINALI YA FIRST LEAGUE KUPIGWA LEO CHAMANZI.

 

MCHEZO wa Fainali wa Ligi ya First League unapigwa leo April 5 kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ukizikutanisha timu za Hausung kutoka Njombe na Gunners ya Dodoma.

Hii inafanyika kwa mara ya kwanza tangu maboresho ya kanuni ya First League kufanyika kwa msimu 2024/25 ambapo hapo awali Bingwa alikuwa akipatikana kwa timu nne za juu kila kundi kucheza shindano dogo la nane bora na timu zikipangwa kwenye makundi mawili yenye jumla ya timu nne na vinara wa kila kundi hucheza mchezo wa nusu fainali na fainali na hatimaye Bingwa kupatikana.

Ikumbukwe kuwa timu hizi tayari zimekwisha kata tiketi ya moja kwa moja kushiriki Ligi ya Championship ya NBC kwa msimu wa 2025/2026 kwa kuongoza makundi yao.

KASEJA AIFUFUA UPYA KAGERA SUGAR

TIMU ya Kagera Sugar imeanza kujipata katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC baada ya kushinda mechi tatu walizocheza hivi karibuni chini ya uongozi wa Kocha wao mpya Juma Kaseja ambaye pia ni golikipa aliyecheza kwa mafanikio makubwa timu ya taifa na timu mbalimbali za Ligi Kuu .

Kaseja ambae alichukua mikoba kutoka kwa Kocha Melis Medo ambae ametimkia katika timu ya Singida Black Stars  aliiongoza timu yake katika mchezo miwili huku mchezo wa kwanza  dhidi ya Pamba Jiji  alifanikiwa kushinda mabao 2-1.

Mchezo mwingine ulichezwa jana April 3 alifanikiwa kuifunga timu ya Coastal Union kwa mabao 2-1 ambapo mabao ya Kagera Sugar yalifungwa na Ally Msangi wa Coastal Union aliyejifunga bao  dakika ya 59 na Mohamed Jecha dakika ya 90  huku mchezaji Lucas Kikoti akiipatia Coastal Union bao dakika ya 84 ya mchezo huo.

Kagera Sugar imefikisha alama 22 ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo baada ya kucheza michezo 24 wakifunga mabao 20 na kufungwa mabao 32.

KEN GOLD ‘HALI TETE’ LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya KenGold kutoka mkoani Mbeya imeendelea kujiweka kwenye wakati mgumu wa kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 baada ya kupoteza mchezo wa 14 wa ligi hiyo msimu huu dhidi ya Azam kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

KenGold inayoshika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC imepoteza mchezo wa 14 msimu huu na kuwa timu iliyofungwa michezo mingi sawa na timu ya Prisons ya Mkoani Mbeya pia.

Mabao ya Gibril Sillah na Nassor Saadun yalitosha kuipa Azam alama tatu muhimu huku golikipa Zuber Foba akimaliza mchezo bila kuruhusu bao na kufikisha idadi ya hati safi ‘Cleansheet’ ya tano msimu huu.

Azam imeendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu ikifikisha jumla ya alama 51 ikizidiwa alama sita pekee na Simba inayoshika nafasi ya pili na alama 10 nyuma ya kinara Yanga.

JKT YASHINDWA KUTAMBA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya JKT Tanzania yenye ‘maskani’ yake uwanja wa Isamuhyo, Dar es Salaam imeshindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na timu ya Dodoma Jiji.

Pamoja na kutangulia kupata bao kupitia kwa nahodha wake Edward Songo JKT ilishindwa kuizuia Dodoma iliyokuwa ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara na kusawazisha mara zote JKT ilipotangulia kwa uongozi.

Mwana Kibuta aliinyima JKT uongozi hadi mapumziko baada ya kusawazisha bao la Songo zikiwa zimesalia sekunde chache kabla ya mapumziko.

Songo aliongeza bao la pili dakika ya 66 na kuipa JKT uongozi uliodumu kwa dakika 15 pekee kabla ya Paul Peter kuisawazishia Dodoma Jiji na kufanya matokeo kuwa 2-2 hadi mwisho wa mchezo.

Matokeo hayo yanaifanya JKT kushika nafasi ya sita na kuwa mbele ya Dodoma inayoshika nafasi ya saba kwa tofauti ya alama tatu.

LIGI KUU NBC ‘KUCHANJA MBUGA’ VIWANJA VITATU,CHAMPIONSHIP MAMBO YAZIDI KUWA MOTO.

MZUNGUKO wa 24 wa Ligi Kuu ya NBC utaendelea kushika kasi  ambapo michezo mitatu itachezwa katika mikoa ya Kagera,Dar es Salaam na Mbeya hivyo kufanya mbio za ubingwa kuzidi kufikia mahali patamu zaidi kwani mmoja anapambana angalau apate alama  ili aweze kubeba ubingwa ama aendelee kubaki msimu ujao .

JKT Tanzania ambayo ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC itakuwa mwenyeji wa Dodoma Jiji  iliyopo nafasi ya nane katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo  uliopo Mbweni Dar es Salaam majira ya saa kumi jioni.

KenGold iliyopo nafasi ya 16   katika msimamo wa Ligi Kuu  ya NBC itakawakaribisha timu ya Azam katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya majira ya saa kumi jioni huku Kagera Sugar atakuwa mwenyeji wa Coastal Union katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera majira ya saa moja usiku.

Kwa upande wa Ligi ya Championship ya NBC timu ya Songea United itaikaribisha timu Biashara United katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma majira ya saa kumi jionI ikiwa ni mzunguko wa 25 wa Ligi hiyo.